Pakua App Yetu Playstore Bofya Hapa!

XMANUAL&WRITINGS

GREENHOUSE CROP PRODUCTION I Mshindo Media

UZALISHAJI WA MAZAO KWENYE NYUMBA YA WAVU YAANI GREENHOUSE

UZALISHAJI WA MAZAO KWENYE NYUMBA YA WAVU YAANI GREENHOUSE

Kilimo cha nyumba ya wavu (greenhouse) kinaendelea kupata umaarufu nchini na ujenzi huu ambao hutumia plastiki au wavu umekuwa chaguo la baadhi ya wakulima kwa sasa nchini.

Hivi sasa kumekuwa na uhamasishaji mkubwa wa kilimo hiki kwa vile wakulima wengi wamekuwa na shauku ya kupata faida kubwa lakini kwa bahati mbaya sana hawana uzoefu wa kutosha wa teknolojia hii. Makampuni mengi yanayojihusisha na uundaji wa greenhouse wanasema kilimo hiki ni kama vile mgodi wa mpya madini kwa maana kwamba hutoa fursa nyingi za faida kibiashara ambapo hakuna mkulima yeyote ambaye angependa kuzikosa.

Ni kweli mtu mwingine anaweza akaangalia teknolojia hii kwa mtazamo tofauti lakini bila shaka teknolojia hii ya kilimo ina faida lukuki kama ifuatavyo:

• Husaidia kulinda mazao ya mbogamboga dhidi ya mvua kubwa na upepo mkali.

• Ndani ya nyumba hii (greenhouse) kiwango cha joto kwa kawaida hupanda kila baada ya muda fulani kulingana na hitaji la hatua fulani ya zao husika hali ambayo hupelekea mazao kukua kwa haraka na kuvunwa mapema kuliko mazao yanayooteshwa nje mashambani.

• Ndani ya miundombinu hii kwa kawaida umwagiliaji wa kutumia mirija (Drip Irrigation) hutumika na hivyo husaidia kuokoa kiwango cha maji kitumikacho, na hufanya uzalishaji wa mazao usiwe wa kutegemea mvua.

• Mkulima huweza kupanda na kuvuna mazao yake kipindi ambacho bei ya zao husika ipo juu

• Kwa kutumia mipango mizuri upo uwezekano mkulima kurudisha gharama alizowekeza ndani ya miaka miwili hadi mitatu.

 

CHANGAMOTO

Hata hivyo mkulima inapasa afahamu kwamba faida za uzalishaji huu zilizoainishwa hapo juu hazidondoki kutoka peponi, kuna changamoto kuu tatu ambazo itambidi kukabiliana nazo kikamilifu hizi ni :

 

GHARAMA

Mkulima anahitaji kuwa na mtaji wa kuanzisha aina hii ya kilimo au kuwa na dhamana ambayo itamwezesha kupata mikopo kutoka benki na taasisi zingine za fedha, kwa bahati mbaya wakulima wengi wadogo hawana uwezo wa yote mawili na ndiyo maana katika nchi yetu wananchi wengi wanachukulia kilimo hiki ni cha watu matajiri au wale hadhi ya kati ambao wengi ni wale wenye ajira za kuwapatia kipato cha uhakika kuumudu gharama za mwanzo.

NAMNA MAZAO YANAVYOSTAWI NDANI YA GREENHOUSE
NAMNA MAZAO YANAVYOSTAWI NDANI YA GREENHOUSE

USIMAMIZI WA UHAKIKA:

Kwa vile uoteshaji na ukuzaji wa mazao ndani ya miundombinu hii hufanyika kwa kudhibiti hali za hewa zinazohitajika hivyo uzalishaji wa mazao kwa njia hii unahitaji udhibiti mkubwa wa kiwango cha joto na unyevu ili kuhakikisha havibadiliki kwa muda wote. Kwenye miradi
mikubwa udhibiti huu hufanyika kwa kutumia vifaa maalum vya teknolojia ya juu ambavyo mkulima mdogo hawezi kuumudu kuwa navyo.

Hivyo kwa wakulima wadogo wanahitajika kuwepo muda mwingi ndani ya miundo hii ili kuhakikisha kiwango cha joto na unyevu unakuwa kama inavyohitajika wakati wote.

Miundo ya namna hii inakuwa ni rahisi kupata joto kubwa wakati wa jua kali hivyo ni vema kuhakikisha unyevu unadhibitiwa. Hii huweza
kudhibitiwa kwa kuruhusu mapitisho ya hewa (ventilation) za kutosha ambayo pia inapasa iwe ni rahisi kiuendeshaji. Hivyo ni muhimu kwa
mikoa ambayo kiwango cha joto huwa cha juu na hivyo kusababisha joto ndani ya miundo hii huwa kikubwa zaidi ya kile kinachohitajika kwa mazao kuweza kukua vyema

• Vilevile ni vema kuwa na wafanyakazi wa uhakika na wenye ufahamu wa kutosha kuendesha kilimo cha hiki na uwezo wa kukabiliana na
changamoto zozote zinazoweza kutokea wakati wa uzalishaji.

 

UDHIBITI WA MAGONJWA NA WADUDU:

 Hii inaweza kuwa ni changamoto kubwa kwa uzalishaji huu. Ili kurudisha gharama kubwa za uwekezaji mazao kama nyanya, pilipili, bilinganya na pilipili hoho huweza kupandwa. Kwa bahati mbaya mazao haya yapo kwenye familia moja ambayo kitaalamu hujulikana kama Night shade family ambayo hushambuliwa kirahisi na aina za kuvu zijulikanazo kitaalamu kama Early blight na Late blight na vilevile upo uwezekano wa vijidudu vingi vya magonjwa huweza kuzaliana kwa wingi ndani ya miundo hii na hivyo kuwa vigumu kama siyo kushindikana kabisa kuwadhibiti.

• Kudhibiti hali hii ni vema wakulima wanaotumia hali hii wakashauriwa kutumia kilimo cha kubadilisha mazao (crop rotation). Hii itaepusha wadudu na magonjwa wanaoshambulia mazao au familia fulani ya mazao kuzaliana ardhini. Lakini pale mkulima atapoamua kupanda mazao ya familia fulani kwa misimu yote bila kubadilisha wadudu na magonjwa huwa ni janga kubwa kwani mara baada ya msimu wa pili na wa tatu wa uzalishaji mavuno yale ya uhakika yaliyokuwa yakipatikana kipindi chote hiki cha mwanzo huanza kupungua kadiri wadudu wanavyozidi kuongezeka na hii hupelekea kuanguka kabisa kwa uzalishaji hali inayopelekea wakulima wengi kubomoa miundo hii. Kwa kutarajia uwezekano wa majanga kama haya kutokea ndiyo maana Makampuni makubwa yanayojihusisha na ujenzi wa miundo hii hupendelea kutoa shauri na mafunzo kwa wateja wao.

• Kwa kutumia ubadilishaji wa mazao mazao yanayopendekezwa kulimwa ndani ya miundo hii zaidi ya jamii ya night shade (nyanya, pilipili, pipipili hoho), ni kama vile jamii ya matango, matikiti maji, passion, brokoli, bamia, viazi mwitu, spinachi, jamii ya kunde, vitunguu swaumu nakadhalika.

• Usimamizi mzuri hujumuisha utumiaji wa kabila za mazao ambayo yana ukinzani dhidi ya wadudu na magonjwa vilevile kutumia viuadudu vya kibaolojia kama vile muarobaini, pareto na tephrosa na viuadudu vya kemikali kama vile Funco, Tebufarm, Safarm,Piricarb, na nyinginezo.

....................................................................................................

About Veterinary Centre&Animal Care

0 comments:

Post a Comment

Powered by Blogger.